Friday, January 18, 2013

TATHMINI YA KUNDI kwa KUNDI!


Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2013, yanaanza huko Nchini Afrika Kusini Jumamosi Januari 19 kwa Mechi ya ufunguzi ya Kundi A kati ya Wenyeji Afrika Kusini na Cape Verde kwenye Uwanja wa Taifa Mjini Johannesburg.
IFUATAYO NI TATHMINI YA KILA KUNDI:
**FAHAMU: KILA KUNDI LITATOA TIMU 2 KUTINGA ROBO FAINALI.
KUNDI A:
-Afrika Kusini
-Cape Verde
-Morocco
-Angola
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Wenyeji Afrika Kusini, wakishiriki Fainali zao za 8, wametwaa Ubingwa wa Afrika mara moja tu pale Mwaka 1996 walipokuwa pia Wenyeji wa Fainali hizo ambako kwenye Fainali yenyewe waliyotwaa Ubingwa waliichapa Tunisia Bao 2-0 Bao zote zikifungwa na Mark Williams ambae aliwahi kuichezea Wolverhampton Wanderers ya England.
Safari hii, Afrika Kusini, maarufu kama Bafana Bafana, watacheza bila ya Staa wa Everton Stephen Pienaar ambae alistaafu kuichezea Nchi yake Miezi mitatu iliyopita.
Katika Kundi hili, mpinzani mkubwa wa Bafana Bafana anaonekana kuwa Morocco ambao walikuwa Washindi wa Pili wa AFCON 2004 na ambao chini ya Kocha Rachid Taoussi wanaonekana kuimarika huku Uwanjani wakiwategemea Maprofeshenali kadhaa wanaocheza Klabu kubwa Ulaya wakiwemo Karim El Ahmadi wa Aston Villa, Beki wa Udinese Mehdi Benatia na Mchezaji wa Fiorentina, Mounir El Hamadaoui.
Cape Verde, Timu changa inayoshiriki Fainali zao za kwanza kwa kuwabwaga Vigogo Cameroun 3-2 kwenye mchujo, wana Wachezaji kadhaa wanaocheza huko Ureno lakini tegemezi kubwa ni Winga Ryan Mendes, Miaka 22, ambae alifunga Bao 3 kwenye Mechi za Mchujo za AFCON 2013 na ambae aling’ara huko Ufaransa na Klabu ya Le Havre na kuzolewa na Klabu kubwa Lille Mwaka 2012.
Timu ya 4 ya Kundi A ni Angola ambao mara mbili wametinga Robo Fainali za AFCON na kuishia hapo na mashine yao ya Magoli ni Straika wa zamani wa Manchester United, Manucho, ambae ana rekodi ya kufunga Bao 21 kwa Mechi 38 za Angola.
Manucho anazo Bao 6 kwa Klabu yake ya sasa ya Spain, Real Valladolid, zikiwamo Bao 2 alizoipiga Real Madrid walipokutana Mwezi uliopita.
KUNDI B:
-Ghana
-DR Congo
-Niger
-Mali
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Bila shaka Ghana, moja ya Timu inayopewa nafasi kubwa kutwaa AFCON 2013, ndio wanaopewa nafasi kubwa kuwa Nambari Wani kwenye Kundi hili na wamesheheni Majina makubwa kama kina Asamoah Gyan, John Pantsil na John Mensah lakini pia watawakosa Mastaa wengine, kina Michael Essien, Sulley Muntari na Andre Ayew, ambao wamefyekwa toka Kikosini na Kocha James Kwesi Appiah.
Mali na Congo DR ndizo zinazotegemewa kuchuana ili kupata nafasi moja kuungana na Ghana kwenye Robo Fainali na zote zina Mastaa maarufu huku Mali ikiwa nao Modibo Maiga wa West Ham na Samba Diakite wa QPR lakini watamkosa Nahodha wao wa zamani Mahamadou Diarra anaechezea Fulham kwa kuumia.
Hata hivyo, Mali wanae tena Mchezaji Momo Sissoko, aliewahi kuichezea Liverpool na sasa yuko Juventus, baada ya kutoichezea Mali kwa Miaka miwili.
Congo DR nao wana Mastaa wao lakini atakaebeba jahazi ni Nahodha Tresor Mputu ambae aliwahi kufungiwa Miezi 12 wakati akiechezea Congo kwa kumpiga Refa.
Niger ni Timu ya 4 kwenye Kundi hili na hii ni Fainali yao ya pili kucheza baada ya AFCON 2012 ambayo hawakuvuka hatua ya Makundi na safari hii tena wanakadiriwa kufanya hivyo hivyo.
KUNDI C:
-Zambia
-Ethiopia
-Nigeria
-Burkina Faso
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Kimaandishi, Nigeria wanaonekana kuwa juu kwenye Kundi hili lakini ukweli ni kuwa Kundi hili liko wazi na yeyote ana nafasi ya kusonga.
Nigeria wametinga Fainali za AFCON mara 6 lakini wamechukua Ubingwa mara mbili tu na baada ya kuzikosa AFCON 2012 Nchi hiyo ilimteua Mchezaji wao wa zamani, Stephen Keshi kuwa Kocha.
Keshi ameteua Kikosi mchanganyiko cha Vijana wanaocheza Soka nyumbani na Maprofeshenali kama kina John Mikel Obi na Victor Moses wa Chelsea na Beki wa zamani wa Everton, Joseph Yobo.
Zambia ndio Mabingwa watetezi wa Afrika baada ya kutwaa Taji la AFCON 2012 kwa kuichapa Timu kali Ivory Coast kwa Mikwaju ya Penati 8-7 huko Nchini Gabon na pia wametinga Fainali hizi za AFCON 2013 kwa Mikwaju ya Penati walipoitoa Uganda katika Mechi ya mwisho ya Mchujo.
Tegemezi la Zambia ni pamoja na Mchezaji wa Southampton, Emmanuel Mayuka, Miaka 21, ambae ameichezea Klabu hiyo ya England Mechi 8, 6 akitokea Benchi.
Timu nyingine za Kundi hili ni Ethiopia na Burkina Faso lakini Ethiopia washawahi kuwa Mabingwa wa Afrika mara moja walipotwaa Taji Mwaka 1962 na safari hii Penati ya Dakika ya mwisho ya Mchezaji Adane Girma kwenye Mechi ya mwisho ya Mchujo na Benin ndio imewaingiza Fainali za AFCON 2013.
Matokeo mazuri kwa Burkina Faso kwenye Mashindano haya ya Afrika ni kukamata nafasi ya 4 kwenye Fainali za Mwaka 1998.
KUNDI D
-Ivory Coast
-Togo
-Tunisia
-Algeria
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Wanasema hili ndio ‘Kundi la Kifo!’
Lakini Timu ngumu Ivory Coast, iliyosheheni Masupastaa wa kila aina, watataka kufanya vyema kupita AFCON 2012 ambako walitolewa kwenye Fainali na Zambia kwa Matuta 8-7 na safari hii kutwaa Ubingwa wa Afrika kwa mara ya Pili katika historia yao.
Macho yote yatakuwa kwa Supa Straika Didier Drogba, ambae licha ya mafanikio yake makubwa kwenye anga la Soka, hajawahi kutwaa Ubingwa wa Afrika.
Togo wanatinga kwenye AFCON 2013 wakiwa na habari njema baada ya Nahodha wao Emmanuel Adebayor kufuta msimamo wa kususa kuichezea Nchi yake baada ya Rais wa Nchi hiyo kufanya mazungumzo nae.
Wengine kwenye Kundi hili gumu ni Algeria na Tunisia ambao kila mmoja ashawahi kuwa Bingwa wa Afrika mara moja na Timu zote zina Wachezaji kadhaa ambao wako Ulaya.
Algeria wanatawategemea Kiungo wa Valencia Sofiane Feghouli, Winga wa zamani wa Fulham na Watford, Hamed Bouazza na Staa wa Nottingham Forest, Guedioura.
Nae Kocha wa Tunisia, Sami Trabelsi, licha ya kuwa na Mastaa kadhaa, inaelekea amejitia kitanzi mwenyewe baada ya kumtema Kiungo Nyota wa Atletico Madrid Kader Oueslati na hili huenda likamfanya atimuliwe ikiwa hatafanikiwa kwani Tunisia, ndani ya Miaka minne, washabadilisha Makocha mara 7.

No comments:

Post a Comment