Tuesday, April 30, 2013

FAHAMU MBICHI NA MBIVU YALIYOJIRI JANA KATIKA KESI YA ,MBUNGE WA ARUSHA MJINI GODBLESS LEMA

MVUA nyepesi iliyonyesha kuanzia alfajiri, jana haikuwazui mamia ya wafausi wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kujitokeza kwa wingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakati mbunge huyo alipofikishwa kusomewa shtaka la uchochezi.

Lema ambaye alikamatwa Ijumaa usiku kwa amri ya Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo, na kuwekwa rumande kwa siku tatu, alifikishwa mahakamani saa tatu asubuhi akiwa katika gari dogo lenye vioo vyeusi likiwa na namba za usajili T 818 AJD.

Mbunge huyo alisindikizwa na askari wawili waliovaa suti wakiwa na silaha pamoja na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO).

Ilipofika saa nne, mbele ya Hakimu Devota Msofe, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Elianenyi Njiro, alidai kuwa kesi hiyo ni mpya na inatajwa mara ya kwanza, angeomba asome mashtaka na ipangiwe tarehe nyingine.

Akisoma mashtaka hayo, alidai kuwa Aprili 24, mwaka huu, katika eneo la Freedom Square Chuo cha Uhasibu, Lema alichochea utendaji makosa na kukiuka kifungu 390 na 35 cha kanuni za dhabu sura ya 16 kama ilivyorekebishwa mwaka 2000.

Alitaja shtaka la Lema ni kutamka maneno: “Mkuu wa mkoa anakwenda kwenye ‘send off’, hajui chuo cha uhasibu mahali kilipo wala mauaji ya mwanafunzi wa chuo hiki. Ameshindwa kuwapa pole kwa kufiwa na kusikiliza shida zenu na anasema hawezi kuongea na wanafunzi wasio na nidhamu.” Alisisitiza kuwa maneno haya ndiyo yaliyosababisha kuvurugika kwa amani.

Baada ya kusoma shtaka hilo, aliongeza kuwa kwa upande wao hawana kipingamizi cha dhamana na hivyo hakimu Msofe alimuuliza wakili wa mshtakiwa, Method Kimomogolo, kama ana la kusema.

Kimomogolo alimueleza hakimu kuwa kwa vile maelezo ya shtaka hayaonyeshi kuelekea kwenye kutenda kosa, anaomba mshtakiwa aruhusiwe kujidhamini mwenyewe kwa kuwa ni mbunge wa Arusha, hivyo hawezitoroka.

Hakimu Devota alitaja masharti ya dhamana kuwa ni mdhamini mmoja mwenye kitambulisho na atakaesaini dhamana ya sh milioni moja ambapo Diwani wa Viti Maalumu (CHADEMA), Sabina Francis, aliitwa na Kimomogolo akamdhamini Lema baada ya kukidhi masharti hayo.

Mara baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, hakimu Msofe aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 29 itakapofika kwa ajili ya kutajwa tena.


Hali mahakamani

Lango la kuingilia katika chumba cha mahakama hiyo lilikuwa na askari sita ambapo watatu walivalia mavazi rasmi wakiwa na silaha na wengine wakiwa wanaangalia kila mtu anaekaribia hapo.

Askari wengine waliovalia kiraia walikuwa ndani ya chumba cha mahakama wakiratibu kila mtu aliyekuwemo ndani ambapo wengi waliokuwamo ni madiwani wa CHADEMA na waandishi wa habari.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, alikaa na Lema wakibadilishana mawazo juu ya kilichotokea.

Nje ya mahakama ambako wananchi wengi walikuwa wamekusanyika, nako kulikuwa na askari wengi waliokuwa wamevalia kiraia.

Mbali na askari kanzu kujaa mahakamani hapo pia askari waliovalia sare wakiwa na gari tano huku wakisheheni silaha nzito pamoja na mabomu ya machozi walifanya doria mahakamani na maeneo ya barabara zote za kuelekea na kutoka eneo hilo.

Kulikuwa na magari yenye namba za usajili PT 2077, PT 1076, PT 2017 na PT 1844, zote zikiwa na askari wenye silaha kati ya saba na tisa wakizunguka maeneo yote jirani na Mahakama Kuu mjini Arusha wakati katika Kituo Kikuu cha Polisi kuliimarishwa ulinzi ambapo hakuna gari lililokuwa likiruhusiwa kuingia.
e
Lema ahutubia

Baada ya kesi kuahirishwa, wafuasi wa Lema waliandamana naye kutoka katika viwanja vya mahakama na kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa wakishangilia hadi ofisi za CHADEMA mkoa.

Kutokana na wingi wa wafuasi hao ililazimu Lema kuzungumza nao katika kiwanja cha Shule ya Msingi Ngarenaro.

Aliwashukuru kwa kujitokeza kumuunga mkono na kuwasihi kuwa kamwe wasiwe waoga katika kutetea haki zao mpaka wahakikishe nchi inakombolewa.

Pia Lema alivishukuru vyombo vya habari kwa kuripoti ukweli halisi wa tukio na kusaidia kuepuka kubambikiwa mashtaka.

Alisema licha ya kuwekwa rumande lakini imemsaidia kujua masahibu mengi wanayoyapata mahabusu wanapokuwa sero, kwamba kuna mahabusu wana siku 26 hadi 40 hawajafikishwa mahakamani.

Alisema ameshangazwa kukuta chumba cha kukaa watu 20 wanalazwa watu 90 kitendo ambacho alidai kinahatarisha usalama wa mahabusu.

Lema alisema kuwa hatokwenda bungeni wiki yote ili apate muda wa kufanya mikutano ya hadhara huku akiwasisitizia wananchi wa Arusha mjini kumzomea mkuu wa mkoa popote atakapokwenda.

“Nasisitiza ilikuwa ni haki yake kuzomewa na wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu kutokana na dharau alizozionyesha alipofika chuoni hapo na nawaambia wakazi wa Arusha kuendelea kumzomea popote atakapokwenda jimboni kwangu,’’ alisema.

Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na MJUKUU WA TOZO baada ya Lema kuachiwa walimlalamikia mkuu wa mkoa wakisema ametumia madaraka vibaya pamoja na kumpotezea muda Lema wakati shtaka lenyewe halina mashiko.

Walisema kuwa ifike wakati uwekwe utaratibu wa kuwadhibiti viongozi kama hao wanaochezea kodi za wananchi kwa mambo yasiyo na msingi.

Naye Nasari alimuonya Mulongo kuacha tabia ya kuwadharau wabunge wa CHADEMA na kusema hali hiyo itamfanya ashindwe kuongoza mkoa huu.

Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, mbali na suala hilo la Lema alitoa tamko la chama kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia kwa Mkurugenzi wa Jiji kuiunganisha kata ya Sombetini katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Juni 16.

Monday, April 29, 2013

LEMA AACHIWA KWA DHAMANA


wafuasi wa chadema wakiwa wanasubiria hukumu ya Mbunge wao nje ya mahakama kuu ya Arusha


Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema ameachiwa kwa dhamana ya sh. milioni moja  baada ya kushtakiwa kwa makosa ya uchochezi katika mahakama ya Mkoa wa Arusha huku maandamano yakifanyika  katika mitaa ya Jiji la Arusha.

Kesi ya uchochezi dhidi ya Lema imefunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Arusha na inaendeshwa na Hakimu Devota Msoffe

Kesi  hiyo imeahirishwa mpaka Mei 29 mwaka huu huku Katika hati ya mashtaka ambayo ipo katika mahakama hiyo inasema kwamba kosa la Lema ni  kutoa maneno yanayodaiwa kuwa ni uchochezi.




Baada ya hukumu hiyo mashabiki, wafurukutwa na wanachama wa Chadema wamefanya maandamano makubwa kuelekea katika ofisi za chama hicho ambazo zipo katika eneo la Ngarenaro mkoani humo.

Saturday, April 27, 2013

Mambo yaliyomfanya Mbunge wa arusha Godbless Lema akamatwe na kunyimwa dhamana jana

Mambo yaliyomfanya Mbunge wa arusha Godbless Lema akamatwe na kunyimwa dhamana jana ni haya yafuatayo baada ya kuongea na Mwanasheria wa Lema wakili Humphrey Mtui

i)Kosa la kwanza ni kuwaambia wanafunzi wa chuo cha uhasibu alipoenda kuwatuliza kuwa ‘dhambi kubwa kuliko zote ni woga ‘.Haki hutafutwa na kupiganiwa ikiwa jambo unalipigania ni la msingi na linafaa kupiganiwa(Worth fighting for)

ii)Kosa la pili ni pale alipotamka kuwa ‘’Tumemtafuta mkuu wa mkoa juu ya Matatizo yenu na mlivyoshuhudia hapa amechukua muda mrefu na kuingia kama vile anaingia kwenye send-off.Hawa ndiyo viongozi wetu ambao hawajali matatizo ya wananchi’’Kwa hiyo huo ni uchochezi

iii)Kosa la Tatu ni pale alipotamka kuwaambia wanafunzi kuwa ‘’Mimi Mbunge wenu nipo sambamba nanyi hadi mpate haki yenu na ikiwa mkuu wa mkoa hatakuja hapa kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi wa mkoa nitawaongoza hadi ofisini kwake ili mpate majibu na haki yenu kwani ni haki yenu ya msingi kwa mujibu wa katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ambayo niliapa kuilinda Bungeni na pia inaruhusiwa kwa mujibu wa kikanuni na kifalsafa katika utekelezaji wa utawala bora wa kidemokrasia ambao msingi wake ni kusikilizwa na kulinda haki za binadamu’’Huu nao umeitwa kwamba ni uchochezi.




Friday, April 26, 2013

FAHAMU KUHUSU KUKAMATWA KWA GODBLESS LEMA..SASA KUFIKISHWA KIZIMBANI JUMATATU















MAMBO yamezidi kumwendea kombo Mbunge wa Arusha Mjini, (Chadema) Godbless Lema baada ya Jeshi la Polisi kutangaza rasmi kwamba itamfikisha Mahakamani, siku ya Juma tatu.
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa ArushaLiberatus Sabas amema kwamba Mbunge huyo hawezi kuachilia huru kwa sababu mashtaka dhidi yake yameshakamilika na atafikishwa Mahakamani siku ya Juma tatau.
"Hatuwezi kumwachia kwa sababu anatarajia kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili"alisema Sabas.
Wakati Kamanda huyo akitoa msimamo huo, taarifa za ndani ya Jeshi hilo zinaeleza kwamba Mbunge huyo amehojiwa kwa zaidi ya saa nane sasa na bado yuko katika chumba maalum kwa mahojiano zaidi na maofsa wa Polisi huku akitakiwa kuonyesha ujumbe mfupi wa vitisho aliyodaiwa kuwa ametumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo.

Katika hatua nyingine Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Arusha, kimekuwa na kikao kirefu kinachoongozwa na Mkuu wa Mkoa Mulongo na kwamba ajenda kubwa inayojadiliwa ni tukio zima la vurugu zilizotokea katika Chuo cha Uhasibu mkoani humo. Lema alikamatwa usiku wa kuamkia leo baada ya Askari wa Jeshi la Polisi kumfuata nyumbani kwake na kuzingira nyumba yake kabla ya zoezi la kumchomoa ndani ya nyumba hiyo kufanyika.
Mbunge huyo anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kosa la kuchochea vurugu katika chuo hicho baada ya kutokea mauaji ya Mwanafunzi Henry Koga aliye uawa kwa kuchomwa kisu juzi akirejea chuoni hapo kutoka kwenye matembezi yake, hata hivyo haijajulikana mara moja sababu za kuawa kwa mwanafunzi huyo wala watuhumiwa hawajakamatwa.

Lema: RC amenitumia ujumbe wa vitisho

 Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amedai kupokea ujumbe wa vitisho kwa simu kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Lema alidai kuwa ujumbe huo umeandikwa kupitia simu ambayo namba 0752960276 na unaosomeka: “Umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi.”

Alisema baada ya kupata ujumbe huo, alimjibu kuwa “nimekupata nimekuelewa nipo tayari kwa lolote.”
Hata hivyo, Mulongo amekana kumtumia Lema ujumbe huo... “Nimepata hizi taarifa wewe ni kama mtu wa nane kuniuliza. Sijatuma huo ujumbe na siwezi kuwa na mawazo ya kumtumia ujumbe huo kwani kama ningetaka kumkamata tangu jana pale Chuo cha Uhasibu ningemkamata.”

Hata hivyo, alihoji sababu za mbunge huyo kujificha kama anajijua kwamba hana kosa. “Kwanza nani kamwambia anataka kukamatwa? Yeye anatakiwa kusaidia polisi, kwani wale vijana 13 waliokamatwa kwa ajili yake wapo mahabusu anasubiriwa atoe maelezo.”
kuwa na mawazo ya kumtumia ujumbe huo kwani kama ningetaka kumkamata tangu jana pale Chuo cha Uhasibu ningemkamata.”

Hata hivyo, alihoji sababu za mbunge huyo kujificha kama anajijua kwamba hana kosa. “Kwanza nani kamwambia anataka kukamatwa? Yeye anatakiwa kusaidia polisi, kwani wale vijana 13 waliokamatwa kwa ajili yake wapo mahabusu anasubiriwa atoe maelezo.”
Alisema Mbunge huyo, anajua kazi ambayo, ilifanya chuo cha uhasibu na ndiyo sababu anajificha... “Alifanya kazi yake nikazomewa, kama ningetaka kutumia madaraka yangu asingekuwa salama … nadhani Lema anahitaji kusaidiwa ili abadilike.”

Kuhusu madai ya kujificha, Lema alisema haitajisalimisha polisi licha ya Mulongo kuagiza akamatwe kwa kuwa kuna taratibu za kufuatwa polisi inapomhitaji mbunge ambaye amechaguliwa na watu.
Alisema kama polisi wanamuhitaji, wanapaswa kumuita na pia kuwasiliana na Ofisi ya Spika wa Bunge.
“Naomba ieleweke kuwa mimi sijawakimbia polisi, siogopi kesi na wala siogopi jela nitaendelea na shughuli zangu waje kunikamata barabarani,” alisema Lema.

Akizungumzia tukio la juzi, Lema alidai kuwa mkuu huyo wa mkoa ndiye aliyekuwa chanzo cha vurugu kwa kukosa weledi wa kuzungumza na wanafunzi wenye majonzi.
Alisema alikwenda chuoni hapo baada ya kuitwa na wanafunzi na kabla ya kuzungumza, alikutana na uongozi wa chuo, akiwamo Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Arusha.
“OCD Arusha aulizwe kazi ambayo nilifanya kutuliza hasira za wanafunzi na tutasambaza DVD zaidi ya 3,000 kwa wakazi wa Arusha kujionea tukio hili ambalo sasa limebadilishwa na kuwa la kisiasa,” alisema Lema.
Mwanafunzi, Henry Kago(22) aliyeuawa kwa kuchomwa kisu na watu wasiojulikana na kusababisha wanafunzi kucharuka chuoni hapo anatarajiwa kusafirishwa leo kwenda Iringa kwa mazishi.

ISOME TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA KWA MH.LEMA





Jana majira ya saa nne asubuhi nilipokea taarifa kutoka Chuo cha Uhasibu juu ya tukio la mauaji ya mwanafunzi yaliyotokea jana usiku kwa kuchomwa kisu eneo karibu na chuo , nilipita Chuoni hapo baada ya kusikia taarifa hiyo , nilikuta Wanafunzi wengi sana wakiwa wamekusanyika pamoja wakiwa na jazba huku Kamanda wa Jeshi la Polisi Wilaya akijaribu kuwasihi watulie wakati walipokuwa wanatafuta muafaka wa kuzuia jazba ambayo ilikuwa ina lengo la kuandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa.

Nilipata faragha ya kuongea na Mwalimu aliyekuwa pale ( Dean of Student ) pamoja na OCD na wote walinieleza tatizo lilivyoanza na kuomba nitumie busara kuzuia jazba na maandamano hayo yaliyokuwa yamepangwa kuelekea kwa Mkuu wa Mkoa niliongea na wanafunzi na niliwasihi watulie na nilifanya jitihada za kumtafuta Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa na kwa bahati nzuri nilimpata Mkuu wa Mkoa na kumweleza juu ya kifo hicho na kile ambacho wanafunzi wanakusudia kufanya kuandamana kwenda ofisini kwake. Nilimuomba afike ili aweze kutuliza hali hile na pia atoe kauli juu ya tukio hilo baya la kuhuzunisha kwani ikizingatiwa kuwa ni zaidi ya mara moja matendo kama haya yamekuwa yakitokea na hakuna hatua zozote zimekuwa zikichukuliwa kuwahakikishia Wanafunzi Usalama wao na mali zao.

Mkuu wa Mkoa pamoja na mimi kumpa taarifa mapema aliahidi kufika mapema jambo ambalo halikufanyika na wanafunzi walianza kuwa wakali na nilifanya jitihada na hekima za hali ya juu kuvuta subira za wanafunzi hao ili Mkuu wa Mkoa afike . Baada ya Mkuu wa Mkoa kufika Makamu wa Chuo aliniomba niwaandae wanafunzi kumsikiliza Mkuu wa Mkoa na yeye alikwenda kumchukua Mkuu wa Mkoa na kumpa mukutasari wa tukio zima na hali halisi ya kilichokuwa kinaendelea na kimsingi Mkuu wa Mkoa alipofika Wanafunzi walitaka apande juu kuongea mahali ambako tulitumia kama jukwaa kwa maongezi wakati wote lakini badala yake mambo yafuatayo yalianza kutokea 

1) Mkuu wa Mkoa alikataa na kunitaka nishuke chini mahali alipokuwa yeye na timu yake ya ulinzi na usalama Mkoa kwa kweli nilitii na nilipotaka kuongea nae alinidharau na kuniambia hawezi kuongea na wanafunzi wahuni wasiokuwa na nidhamu maneno ambayo yaliwatia wanafunzi hasira zaidi na nilimsihi na kumuomba Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa (RSO) kumshawishi Mkuu wa Mkoa kukubali kuongea nao kwani hali ilivyokuwa ni dhahiri kwamba wanafunzi wale walikuwa na jazba ya hali ya juu na hivyo hekima na unyenyekevu ndio ilikuwa njia pekee ya kutuliza hali hile. 

2) Mkuu wa Mkoa alitoa masharti kwamba asingeweza kuongea nao bila kipaza sauti na wanafunzi wote waende jengo lililokuwa karibu na Utawala na wakisha kaa atakuja kuongea nao jambo ambalo wanafunzi waligoma kwa imani kwamba jengo hilo lisengeweza kuchukua wanafunzi wengi na mimi niliaga naondoka kwenda msibani na wanafunzi waligoma nisiondoke mpaka watakapo sikilizwa na kwa kweli nilitii maombi baada ya kunizuia na kukaa mbele ya gari yangu.

3) Tulipokwenda eneo la kukutania na mara hii ilikuwa ni nje jirani ya jengo la utawala wanafunzi walikusanyika wakimsubiri Mkuu wa Mkoa na kabla hajafika nilitwa na yeye mwenyewe ili tuweke msimamo wa pamoja kama viongozi lakini badala yake alitumia Polisi kunitisha na kuhaidi kuwa nitamtambua kuwa yeye ni Serikali ,tulitofautiana tena nilipokataa hofu hiyo na ghafla tuliamua kwenda eneo la kuongea na wanafunzi na ndipo yafuatyo yalitokea “

Mkuu wa Mkoa wakati anaanza kuongea alianza kusema maneno yafuatayo “ Mnaona hiki Kifua na huu mwili wangu , na hapo ndipo hali ilipochafuka na kuamsha vurugu kubwa kutoka kwa Wanafunzi waliokerwa na kauli yake na Polisi wa walimchukua na tafrani kati ya Polisi na Wanafunzi ikapamba moto hali iliyosababisha mabomu ya machozi kulipuliwa kwa wingi kila kona ya chuo na kila mtu kuanza kukimbia kuangalia usalama wake nikiwemo mimi .
Nimesikiliza Mkutano wake na Waandishi wa Habari na leo nimesoma nakusikiliza vyombo mbali mbali vya habari kwamba ninatafutwa na Polisi kwa amri ya Mkuu wa Mkoa , nimeshangaa sana japo sio kumshangaa Mkuu huyu wa Mkoa kwani ufahamu na uwezo wake naujua ulivyo katika kufikiri na kutatua mambo ya msingi na muhimu , kwa jinsi nilivyomsikia na kumuona alivyokuwa anashughulikia tatizo lile lililotukutanisha jana pale Chuoni , kwa kweli nilishangazwa sana na kuogopa kama hekima ya Mkiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa angeweza kushughulikia tatizo lile kwa namna ile ya Kiburi , Dharau na Majivuno ambayo hakika ilikuwa ni chanzo cha wanafunzi kukataa kumsikiliza na ndipo alipoamua kuondoka huku zomea zomea ikiendelea kushamiri vizuri . Mabomu yalianza kupigwa , wanafunzi walipigwa na kunyang’anywa pesa , simu , na lap top na vitu mbali mbali ambavyo Polisi walikuwa wanaona vina thamani kwao , nilikuwa ninatazama mambo haya huku roho yangu ikiwa inauma sana kwamba wanaopaswa kulinda usalama wa raia na mali zao ghafla waligeuka kuwa vibaka wa kuumiza raia na kupora mali zao .

Ninawapa pole wanafunzi kwa msiba wa rafiki yao na siku ya jana ilikuwa ni siku ya Serikali kutumia busara kurudisha matumaini kwa wanafunzi wale pamoja na raia , lakini badala yake wafiwa walipotaka kudai haki zao za kulindwa , walipigwa , walidhalilishwa na Chuo chao kufungwa bila sababu ya msingi wala kuzingatia mambo muhimu .

Ifahamike kuwa Chuo cha Uhasibu Arusha kina wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za nchi hii, na amri ya mkuu wa mkoa kufunga chuo na kuamuru wanafunzi watawanyike ifikapo saa kumi na mbili jioni , huu ni ukosefu wa upendo , hekima , busara na utu ikizingatiwa kuwa sababu na mchochezi wa vurugu hizi ni Mkuu wa Mkoa kukosa maarifa na hekima.

Nimepokea ujumbe katika simu yangu kutoka kwenye simu yangu ya kiganjani kutoka kwa Mkuu wa Mkoa inayonitishia na kuweka maisha yangu kwenye hali ya hatari na ujumbe huo unasema “ UMERUKA KIHUNZI CHA KWANZA , NITAKUONYESHA KUWA MIMI NI SERIKALI ULIKOJIFICHA NITAKUPATA NA NITAKUPA KESI NINAYOTAKA MIMI “ Mwisho wa kunukuu .

Mwisho, Ninamshukuru kijana aliyerekodi tukio lote kuanzia mwanzo mpaka mwisho na hivi tutanza kusambaza video cd hizo Nchi ili watanzania wajue ukweli na Mh Rais aone utendaji mbovu wa wateule wake na vile nilitake Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria , maadili ,taratibu na kanuni za kazi na sio kuendesha Jeshi kwa matakwa ya kisiasa , kufanya hivi ni kuhatarisha usalama na utulivu wa Nchi yetu . 

“ Che Guavera alisema “ if you tremble indignation at every injustice then you are a comrade of mine “ 

Wanafunzi jipeni moyo bado kitambo kidogo Taifa hili litabadilika .


Godbless J Lema ( MP) 


25/4/2013.

KUFUATIA KIFO CHA MWANACHUO ALIYEUWAWA JIJINI ARUSHA CHADEMA CHA TOA TAMKO


chademaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa
TAARIFA KWA UMMA
MAUAJI YA MWANACHUO WA CHUO CHA UHASIBU ARUSHA (HENRY KAGO) NA KAULI YA CHAFU YA MKUU WA MKOA WA ARUSHA
Ndugu wanahabari na wakazi wote wa mkoa wa Arusha.
Kwanza kabisa, tunapenda kutoa pole za dhati kwa familia, ndugu jamaa, wanachuo na jumuia yote ya chuo cha uhasibu Arusha wa marehemu Henry Kago aliyefariki juzi usiku kwenye tukio la kutisha na kuhuzunisha sana.

Tumesikitishwa na msiba huu na tunawaombea wote Mungu awapatie faraja na utulivu katika kipindi hiki kigumu.

Katika tukio hili, mbunge wa Arusha Mjini Mhe Godbless Lema alijulishwa na kama kiongozi alifika ili kuona namna atakavyoweza kutoa msaada hasa baada ya wanachuo kuonyesha hisia zao kwa vile hawakuona kupata msaada kutoka kwa uongozi wa chuo na serikali kwa ujumla. Hili ni tukio la pili la mauaji ya mwanachuo sambamba na matukio mengi ya wanachuo kuvamiwa na kunyang’anywa mali zao.

Mhe Lema aliwatuliza wanachuo na kuchukua hatua za kumjulisha mkuu wa Mkoa Mhe Mulongo aje na kuzungumza na vijana hawa.

Hata hivyo ujio wa mhe Mulongo ulionekana haukuwa na dhamira ya dhati na badala yake alionyesha madharau makubwa ambayo mpaka sasa nashindwa kuelewa alikuwa na maana gani kuonyesha tabia ya kipuuzi namna ile kwa vijana waliokuwa wamepata msiba wa mwenzao.

Picha za video zinaonyesha kwa dhahiri jitihada kubwa aliyoifanya mhe Lema kuwatuliza vijana hawa na kuwaomba wawe wavumilivu.

Baada ya tukio zima kukumbwa na vurugu ambazo kimsingi chanzo ni tabia aliyoinyesha Mhe mulongo kwa vijana hawa, mkuu wa mkoa aliongea na waandishi wa habari kuwa chanzo cha vurugu hizo ni Mhe Lema na kuwa tukio zima la mauaji haya ni masuala ya kisiasa na kuwa wanasiasa wamepanga mambo haya ili kujipatia umaarufu, hii na kauli ya mwendawazimu kabisa. 

Katika hatua hii walimkamata Wakili Mhe Albert Msando ambaye pia ni diwani wa CHADEMA na kumchukua kwa mahojiano.

Kwa ujumla msingi wa suala la kumtafuta muuaji wa Henry umepabadilika na kuwa kumtafuta Lema.

Tunataka tuweke kumbukumbu hii kwa wakazi wa Arusha, jambo hili ni mfululizo wa matukio mengi yasiyoonyesha weledi ya Mhe mulongo ambayo amekuwa akifanya na kama chama tunamtakia hivi kikombe kitakopajaa atatambua maana ya nguvu ya umma.

 Anaweza kudharau maneno haya, afanye hivyo kwa vile anajisikia kuwa yupo na mamlaka ya kiserikali lakini tunarudia kusema kuwa kamwe hatuwezi kuendelea kuvumilia uongo na akili mbovu za namna hii kuongoza watu wenye akili. Narudia kusema hatutavumilia uongo wa namna hii kuendelea kusemwa halafu familia iliyopoteza mtoto wao mpendwa ikiwa katika masononeko makubwa.

Sasa mhe Mulongo na watu wake wajiandae vema maana tumejiandaa kupambana na watu na/au viongozi ambao tumeshajua ni wapotoshaji na wahuni na wanafanya mambo ya kihuni.

Tunawaomba wakazi wa Arusha wawakatae viongozi wapotoshaji na wahuni, wasiwape ushirikiano wowote ule na sisi tutasimama na wananchi kwa pamoja katika mazingira yote ili kudumisha uongozi bora wenye kujali na kuheshimu raia wote kwa mustakabali wa mkoa wetu kiuchumi na katika kujenga utulivu.
Imetolewa leo tarehe 25 Aprili 2013
Amani Golugwa
KATIBU WA CHADEMA – KANDA YA KASKAZINI.