Serikali,
kuanzia leo tarehe 01 Agosti, 2012, imewavua hadhi ya ukimbizi wakimbizi 38,050
wa kutoka Burundi wanaohifadhiwa katika kambi
ya wakimbizi ya Mtabila iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma.Uamuzi huu
wa kuwavua hadhi ya ukimbizi umefanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk.
Emmanuel Nchimbi kwa Mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya
Wakimbizi.
Kufuatana na
Sheria hiyo mkimbizi anapoteza hadhi ya ukimbizi kama mazingira yaliyomfanya
kuwa mkimbizi yatakuwa hayapo tena, na atavuliwa hadhi hiyo kama ataendelea
kukaidi maagizo halali ya kumtaka kurejea kwao kwa hiari.
Hatua ya
kuwavua hadhi ya ukimbizi wakimbizi hawa imefikiwa baada ya Serikali za
Tanzania na Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi
(UNHCR) kujiridhisha kuwa hapakuwa tena na sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi hao baada ya hali ya
amani kurejea nchini mwao na hivyo kuwataka kurejea kwao.
Zoezi la
kuwasaili wakimbizi waliopo katika kambi ya wakimbizi ya Mtabila lilifanyika
kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba mwaka 2011 kwa lengo la kubaini kama
walikuwepo wakimbizi wenye sababu za msingi za kuendelea kuwepo nchini, ambapo
ilibainika kuwa wakimbizi 38,050 hawakuwa na sababu za kuendelea kuwa
wakimbizi.
Kufuatia
matokeo ya zoezi hilo, Kikao cha Pande Tatu, kilichojumuisha wawakilishi wa
Serikali za Tanzania na Burundi na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kilifanyika jijini
Bujumbura nchini Burundi tarehe 22 Februari, 2012 na kukubaliana kwa pamoja
kuifunga kambi ya Mtabila ifikapo tarehe 31 Desemba, 2012.
Baada ya
kuwavua hadhi ya ukimbizi, raia hawa wa Burundi sasa wataendelea kusaidiwa
kurejea kwao kwa hiari hadi tarehe 31 Desemba mwaka huu, ambapo Kambi hiyo ya
Mtabila itafungwa rasmi, na wale ambao watakuwa hawajaondoka baada ya tarehe
hiyo watachukuliwa kuwa ni wahamiaji haramu, na kushughulikiwa kufuatana na
Sheria ya Uhamiaji.
Historia ya
hifadhi ya wakimbizi hapa nchini ilianza tangu mwaka 1961 ambapo Tanzania
ilikuwa na idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, idadi
ambayo katika miaka ya tisini ilifikia takribani milioni moja, 641,386 kati yao
wakiwa ni wakimbizi kutoka Burundi.
Zoezi la
kuwarejesha kwao wakimbizi wa Burundi
lilianza rasmi mwaka 2002 baada ya nchi yao kurejea katika hali ya amani na
hadi sasa kambi nane zilizokuwa zikihifadhi wakimbizi toka Burundi zimefungwa.
Kambi hizo ni Karago, Mtendeli, Kanembwa na Nduta zilizokuwa wilayani Kibondo,
na Muyovosi iliyokuwa wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Kambi nyingine
zilizofungwa ni Kitali iliyokuwa wilayani Biharamulo, Lukole A na B zilizokuwa
wilayani Ngara, mkoani Kigoma.Kambi ya wakimbizi ya Mtabila ndiyo itakuwa ya
mwisho kufungwa katika mlolongo wa kambi zilizokuwa zikihifadhi wakimbizi
kutoka Burundi hapa nchini.
source:mwanawamakonda.blogspot.com