Wednesday, July 25, 2012

Rais mpya wa Ghana kuimarisha utulivu.

Bw.John Dramani akiapishwa Mahakamani.


Kiongozi mpya wa Ghana John Dramani Mahama ameahidi kuimarisha hali ya utulivu kufuatia kifo cha Rais John Atta Mills. Bw. Mahama mwenye umri wa miaka 53, aliapishwa saa kadhaa baada ya Rais aliyekuwa na umri wa miaka 68 kufariki hospitalini mjini Accra.


Upinzani wa nchini humo umesifu kasi iliyotumiwa katika kufanya mabadiliko yaliyomkabidhi Bw.Mahama mamlaka ya kuiongoza nchi ya Ghana na kusema kuwa ni kuonyesha kuwa Ghana ina upevu Kidemokrasi.


Bw. Atta Mills aliyeiongoza Ghana kuanzia mwaka 2009 alikua na saratani ya koo na alikua na mipango ya kuwania muhula wa pili katika uchaguzi unaopangwa kufanyika mwezi disemba.


Mwandishi wa BBC mjini Accra, Sammy Darko anasema kuwa Rais aliyekabidhiwa wadhifa wa Rais ataongoza kama Rais hadi wakati wa uchaguzi, ingawa haijafahamika kama atasimama kama mgombea rasmi wa chama cha NDC(National Democratic Congress.)


Wakati wa kuapishwa mbele ya kikao maalum cha Bunge kilichoitishwa kwa dharura, Bw.Mahama aliahidi kuwahudumia raia wote wa Ghana. Punde baada ya kutangazwa kuwa Rais, Bw.Mahama alitangaza maombolezi ya wiki nzima.


Kiongozi wa upinzani wa chama cha New Patriotic Party Nana Akufo Addo amesema ameahirisha kampeni za kugombea kiti cha Rais kwa heshima ya marehemu.


Mwenyekiti wa NPP Jake Obetsebi-Lamptey amesifu jinsi mabadiliko yalivyofanywa kufuatia kifo cha Rais.


Ingawa kulikuepo na mjadala mkubwa kuhusu afya ya Bw.Atta Mills, suala hilo halikugusiwa rasmi, wanaserma wandishi wa habari. Kiongozi huyo alikanusha kuhusu maumivu na kusisitiza kua katika hali nzuri ya afya.


Kulingana na msaidizi wa Rais, marehemu alilalamika kua na maumivu siku ya jumatatu jioni na tangu hapo hali yake ikazidi kua mbaya.

Source:mwanawamakonda.blogspot.com

No comments:

Post a Comment