JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
TAMKO LA SERIKALI
GAZETI LA MWANAHALISI LAFUNGIWA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelifungia
kutochapishwa gazeti la MwanaHalisi kuanzia 30 Julai, 2012 kwa muda
usiojulikana kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za
uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi
kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani na
mshikamano uliopo nchini.
Katika matoleo yake hivi
karibuni, gazeti la MwanaHalisi toleo Na. 302 la Jumatano Julai, 11 –
18, 2012 na toleo Na. 303 la Jumatano Julai 18 – 24, 2012 na toleo Na.
304 la Jumatano Julai 25 hadi 01 Agosti, 2012 na mengine yaliyotangulia
yamekuwa yakichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa
jamii.
Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi, ameitwa na
kuonywa mara nyingi, lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya makala zake
hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya
uandishi wa habari.
Mhariri, mara zote katika utetezi
wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi yetu ambacho
kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi kutonukuu kifungu cha 30
cha Katiba hiyo kinachoweka ukomo wa uhuru.
Uamuzi wa Serikali
Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda
usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya
mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai,
2012 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 258
lililochapishwa katika Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar Es
Salaam tarehe 27 Julai, 2012.
Serikali inawataka
wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na
maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa
kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.
Kama ilivyoelezwa Bungeni wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni waandishi na
watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika
na vipindi wanavyoandaa vinazingatia taaluma na kuweka mbele maslahi ya
Taifa letu na uzalendo. Uhuru na haki ya vyombo vya habari uendane na
wajibu.
Kuanzia sasa Serikali haitasita kuchukua hatua
dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa maksudi vitatoa taarifa za
uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini
mwetu.
Imetolewa na
OFISI YA MSAJILI WA MAGAZETI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO