Tuesday, September 25, 2012

Mzungu aishitaki Yanga Fifa,kuna hatari ikashushwa daraja, Tff nayo yasema haitambui mabadiliko ya sekretariet


Papic kushoto akiwa na BIN ZUBEIRY enzi zake Yanga

Na Mahmoud Zubeiry
ALIYEKUWA kocha wa klabu ya soka ya Yanga ya Dar es Salaam, Kostadin Bozidar Papic amefungua mashitaka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), dhidi ya klabu hiyo, akidai malimbikizo yake ya mishahara, dola za Kimarekani 12,300, zaidi ya Sh. Milioni 15 za Tanzania.   
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah Malabeja ameiambia BIN ZUBEIRY leo mchana kwamba, wamepokea barua kutoka Kitengo cha Sheria cha FIFA, kiwataka tuitaarifu Yanga kuhusu mashtaka yaliyowasilishwa na kocha wao huyo zamani, raia wa Serbia.
Angetile amesema Katika malalamiko yake, Papic anadai kuwa hajalipwa malimbikizo ya mshahara wake yanayofikia kiasi cha dola 12,300 za Kimarekani. Katika barua yake, kocha huyo anadai kuwa alikuwa akiwasiliana na maofisa na viongozi waYanga, lakini hakupata ushirikiano na hivyo kuamua kwenda FIFA.
Angetile alisema TFF ilifanya juhudi za kuwasiliana na Yanga kuhusu malalamiko hayo ili kujaribu kumzuia kocha huyo asishtaki FIFA, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.
“Na kama chombo kinachosimamia uendeshaji wa soka nchini, TFF imesikitishwa na habari hizo na inaiomba klabu ya Yanga kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa inawasilisha taarifa zote muhimu na nyaraka zinazohusiana na stahiki za kocha huyo ili kama ilishamalizana naye, sifa ya klabu ya Yanga isafishwe,”alisema Angetile.
Alisema tayari wamekwishaiandikia barua Yanga kuitaka itekeleze utashi huo mapema iwezekanavyo.
“Tukio hilo, si tu linachafua sifa ya klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la malipo ya makocha nchini, ni dhahiri kuwa itakuwa ni vigumu kwa klabu zetu na hata timu za taifa kupata makocha wazuri kutoka nje kwa kuwa watakuwa wamejengeka hofu ya kufanya kazi nchini,”alisema.
Hili ni tukio la pili kwa Yanga baada ya mchezaji wake mwingine, John Njoroge kuishtaki klabu hiyo FIFA na kushinda kesi yake iliyoamuliwa mwezi Januari na Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro cha FIFA (DRC).
Alisema ushindi wa Njoroge unamaanisha kuwa iwapo Yanga itashindwa kutekeleza kumlipa mchezaji huyo kasi cha Sh milioni 17, inaweza kujikuta katika adhabu ambayo itailazimisha TFF kuishusha daraja; kuinyang’anya pointi kwa kiwango kitakachotajwa na FIFA; kuipiga faini au adhabu zote kwenda kwa pamoja.
“Tunaiomba Yanga itekeleze hukumu hiyo kwa wakati uliotajwa kwenye barua ya FIFA ili kuepuka hatua hizo,  suala la Njoroge ni moja kati ya matukio mengi yanayohusu ukiukwaji wa taratibu za kuvunja mikataba yanayofanywa na klabu zetu.
Kuna malalamiko ya wachezaji wengi dhidi ya klabu zao za zamani kuhusu kutolipwa stahiki zao. Hivyo TFF inatoa wito kwa klabu kujiepusha na vitendo hivyo kwa kuwa vinawanyima haki wachezaji, lakini pia vinachafua sifa ya nchi iwapo wachezaji wanachukua hatua za kwenda kwenye vyombo vya juu,”alisema Wambura.
Aidha, Angetile amesema kwamba wamekuwa wakisoma kwenye vyombo vya habari kuhusu kutimuliwa kwa sekretarieti nzima ya Yanga kutokana na kuonekana kuwa ina udhaifu, lakini taarifa hizo hazijaifikia rasmi TFF.
Alisema kiutaratibu, Yanga inatakiwa iwsasilishe majina ya maofisa watakaofanya kazi na TFF kwa sasa na itakapoajiri sekretarieti ya kudumu, basi itume barua nyingine ya kuwatambulisha watendaji wake.
Alisema kama Yanga itakuwa imeitimua sekretarieti nzima, basi TFF inapokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa kwani pamoja na kwamba si nia ya TFF kutetea watendaji wazembe, lakini klabu hazina budi kufuatilia kwa karibu utendaji wa sekretarieti zao ili isije ikafikia wakati sekretarieti nzima inaondolewa kwa makosa ambayo yangeweza kusahihishwa kama kungekuwa na ufuatiliaji wa karibu.
“TFF imekuwa ikitoa mafunzo kwa watendaji wa klabu ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kwa mintaarafu ya mpira wa miguu na hivyo kuondolewa kwa timu nzima kama hiyo kunamaanisha kuwa ni upotevu wa rasilimali ambayo imetumika kuwapa elimu ya kutenda kazi zao vizuri. TFF ilishafanya kozi ya Event Management kwa ajili ya watendaji wa klabu; semina ya kuangalia upya maazimio ya Bagamoyo kwa watendaji na viongozi na pia kozi ya utawala hivyo haipendi juhudi hizi zipotee kirahisi,”alisema Angetile.
Chanzo Bin Zubeiry blogsspot

No comments:

Post a Comment