MVUA
nyepesi iliyonyesha kuanzia alfajiri, jana haikuwazui mamia ya wafausi
wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kujitokeza kwa wingi katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakati mbunge huyo alipofikishwa
kusomewa shtaka la uchochezi.
Lema ambaye alikamatwa Ijumaa
usiku kwa amri ya Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo, na kuwekwa rumande kwa
siku tatu, alifikishwa mahakamani saa tatu asubuhi akiwa katika gari dogo lenye vioo vyeusi likiwa na namba za usajili T 818 AJD.
Mbunge huyo alisindikizwa na askari wawili waliovaa suti wakiwa na silaha pamoja na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO).
Ilipofika saa nne, mbele ya Hakimu Devota Msofe, Mwendesha Mashtaka wa
Serikali, Elianenyi Njiro, alidai kuwa kesi hiyo ni mpya na inatajwa
mara ya kwanza, angeomba asome mashtaka na ipangiwe tarehe nyingine.
Akisoma mashtaka hayo, alidai kuwa Aprili 24, mwaka huu, katika eneo
la Freedom Square Chuo cha Uhasibu, Lema alichochea utendaji makosa na
kukiuka kifungu 390 na 35 cha kanuni za dhabu sura ya 16 kama
ilivyorekebishwa mwaka 2000.
Alitaja shtaka la Lema ni kutamka
maneno: “Mkuu wa mkoa anakwenda kwenye ‘send off’, hajui chuo cha
uhasibu mahali kilipo wala mauaji ya mwanafunzi wa chuo hiki. Ameshindwa
kuwapa pole kwa kufiwa na kusikiliza shida zenu na anasema hawezi
kuongea na wanafunzi wasio na nidhamu.” Alisisitiza kuwa maneno haya
ndiyo yaliyosababisha kuvurugika kwa amani.
Baada ya kusoma
shtaka hilo, aliongeza kuwa kwa upande wao hawana kipingamizi cha
dhamana na hivyo hakimu Msofe alimuuliza wakili wa mshtakiwa, Method
Kimomogolo, kama ana la kusema.
Kimomogolo alimueleza hakimu
kuwa kwa vile maelezo ya shtaka hayaonyeshi kuelekea kwenye kutenda
kosa, anaomba mshtakiwa aruhusiwe kujidhamini mwenyewe kwa kuwa ni
mbunge wa Arusha, hivyo hawezitoroka.
Hakimu Devota alitaja
masharti ya dhamana kuwa ni mdhamini mmoja mwenye kitambulisho na
atakaesaini dhamana ya sh milioni moja ambapo Diwani wa Viti Maalumu
(CHADEMA), Sabina Francis, aliitwa na Kimomogolo akamdhamini Lema baada
ya kukidhi masharti hayo.
Mara baada ya kukamilika kwa
taratibu hizo, hakimu Msofe aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 29
itakapofika kwa ajili ya kutajwa tena.
Hali mahakamani
Lango la kuingilia katika chumba cha mahakama hiyo lilikuwa na askari
sita ambapo watatu walivalia mavazi rasmi wakiwa na silaha na wengine
wakiwa wanaangalia kila mtu anaekaribia hapo.
Askari wengine
waliovalia kiraia walikuwa ndani ya chumba cha mahakama wakiratibu kila
mtu aliyekuwemo ndani ambapo wengi waliokuwamo ni madiwani wa CHADEMA na
waandishi wa habari.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, alikaa na Lema wakibadilishana mawazo juu ya kilichotokea.
Nje ya mahakama ambako wananchi wengi walikuwa wamekusanyika, nako kulikuwa na askari wengi waliokuwa wamevalia kiraia.
Mbali na askari kanzu kujaa mahakamani hapo pia askari waliovalia sare
wakiwa na gari tano huku wakisheheni silaha nzito pamoja na mabomu ya
machozi walifanya doria mahakamani na maeneo ya barabara zote za
kuelekea na kutoka eneo hilo.
Kulikuwa na magari yenye namba
za usajili PT 2077, PT 1076, PT 2017 na PT 1844, zote zikiwa na askari
wenye silaha kati ya saba na tisa wakizunguka maeneo yote jirani na
Mahakama Kuu mjini Arusha wakati katika Kituo Kikuu cha Polisi
kuliimarishwa ulinzi ambapo hakuna gari lililokuwa likiruhusiwa kuingia.
e
Lema ahutubia
Baada ya kesi kuahirishwa, wafuasi wa Lema waliandamana naye kutoka
katika viwanja vya mahakama na kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa
wakishangilia hadi ofisi za CHADEMA mkoa.
Kutokana na wingi wa wafuasi hao ililazimu Lema kuzungumza nao katika kiwanja cha Shule ya Msingi Ngarenaro.
Aliwashukuru kwa kujitokeza kumuunga mkono na kuwasihi kuwa kamwe
wasiwe waoga katika kutetea haki zao mpaka wahakikishe nchi
inakombolewa.
Pia Lema alivishukuru vyombo vya habari kwa kuripoti ukweli halisi wa tukio na kusaidia kuepuka kubambikiwa mashtaka.
Alisema licha ya kuwekwa rumande lakini imemsaidia kujua masahibu
mengi wanayoyapata mahabusu wanapokuwa sero, kwamba kuna mahabusu wana
siku 26 hadi 40 hawajafikishwa mahakamani.
Alisema
ameshangazwa kukuta chumba cha kukaa watu 20 wanalazwa watu 90 kitendo
ambacho alidai kinahatarisha usalama wa mahabusu.
Lema alisema
kuwa hatokwenda bungeni wiki yote ili apate muda wa kufanya mikutano ya
hadhara huku akiwasisitizia wananchi wa Arusha mjini kumzomea mkuu wa
mkoa popote atakapokwenda.
“Nasisitiza ilikuwa ni haki yake
kuzomewa na wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu kutokana na dharau
alizozionyesha alipofika chuoni hapo na nawaambia wakazi wa Arusha
kuendelea kumzomea popote atakapokwenda jimboni kwangu,’’ alisema.
Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na MJUKUU WA TOZO baada ya Lema
kuachiwa walimlalamikia mkuu wa mkoa wakisema ametumia madaraka vibaya
pamoja na kumpotezea muda Lema wakati shtaka lenyewe halina mashiko.
Walisema kuwa ifike wakati uwekwe utaratibu wa kuwadhibiti viongozi
kama hao wanaochezea kodi za wananchi kwa mambo yasiyo na msingi.
Naye Nasari alimuonya Mulongo kuacha tabia ya kuwadharau wabunge wa
CHADEMA na kusema hali hiyo itamfanya ashindwe kuongoza mkoa huu.
Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, mbali na suala
hilo la Lema alitoa tamko la chama kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kupitia kwa Mkurugenzi wa Jiji kuiunganisha kata ya Sombetini katika
uchaguzi mdogo utakaofanyika Juni 16.
No comments:
Post a Comment